Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini mkataba wa Makubaliano ya ufadhili wa wanafunzi 1,000 wa Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa ufadhili huo unakwenda kutimiza azma ya Serikali ya kutoa Elimu na Mafunzo yatakayo wawezesha vijana wa kitanzania kupata ujuzi wa kujiajiri ama kuajiriwa.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa mageuzi makubwa ya elimu yanayotarajiwa kutokea, yanatilia mkazo mafunzo ya Amali, hivyo Benki hiyo imekuja wakati muafaka kuiunga mkono Serikali katika mpango huo.
"Tumekuwa tukizungumza mafunzo ya amali sana, tunataka tutoe elimu hiyo inayomwezesha kijana kuwa na ujuzi, leo Benki ya NBC imetushika mkono kwenda hatua moja zaidi ya kufanikisha azma hii," amesema Prof. Mkenda
Aidha Waziri Mkenda amewataka wadau wengine kuiunga mkono Serikali kwenye kuimarisha mafunzo na kuongeza fursa katika Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi - (VETA) na Vyuo vya Kati ili vijana wanufaike na ujuzi utakaopatikana.
Kwa uapnde wake Mkurugenzi Mkuu wa NBC Theobald Sabi amesema kupitia ushirikiano na Wizara, Benki hiyo kwa kuanzia itatoa ufadhili wa Shilingi milioni 100 kwa vijana 1,000 wa VETA kupitia mpango wa " NBC Wajibika Scholarship".
Mkurugenzi Sabi ameongeza kuwa mafunzo yanayo wawezesha vijana kuwa mahiri ndio ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana, na hili si hitaji la Tanzania tu bali kwa Dunia nzima.
"Changamoto ya ajira kwa vijana ni kilio cha Dunia nzima, suluhisho thabiti ni kutengeneza mazingira bora kuwawezesha vijana kujiajiri au kujiendeleza kwa kuwa na ujuzi," alibainisha Mkurugenzi Sabi
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) CPA Anthony Kasore ameishukuru Wizara kwa kuwezesha kupatikana ufadhili huo kutoka Benki ya NBC ambao utawezesha Vyuo hivyo kutoa Mafunzo ya Ujuzi kwa vijana wengi.
Mkurugenzi Kasore amesema kuwa VETA imepokea Mradi huu pamoja na maelekezo ya kuhahakisha zinatumika kwa uwazi na kwa kutoa mafunzo yenye uhitaji na kuleta matokeo chanya kwa haraka.