Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidhi Ameir, ametoa wito kwa wadau wa elimu, wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora na maji safi wakiwa shuleni ili kuboresha afya na kuongeza ufaulu kielimu.



Akizungumza leo Machi 12, 2026 katika maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma, Mhe. Ameir amesema lishe bora kwa wanafunzi ni msingi muhimu wa kujifunza kwa ufanisi.



Mhe, Wanu amesema wanafunzi hutumia muda mwingi wakiwa shuleni, hivyo upatikanaji wa chakula bora, maji safi na mazingira salama ya usafi ni muhimu katika kulinda afya zao na kuongeza uwezo wa kujifunza.



“Kaulimbiu ya mwaka huu inayosema ‘Chakula Bora, Maji Safi Shuleni: Ni Wajibu wa Pamoja’ inatukumbusha kuwa jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora si la Serikali pekee, bali linahitaji ushiriki wa wadau wote,” alisema Mhe. Ameir.



Aidha ametumia fursa hiyo kupongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji unaoendelea kufanyika katika sekta ya elimu ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.



Aidha, alizipongeza taasisi na wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika kuimarisha mpango wa lishe shuleni, akiwemo UNICEF, WFP, Children in Crossfire, GAIN Tanzania, Action Against Hunger pamoja na kampuni ya SANKU kwa mchango wao katika kufanikisha maadhimisho hayo.



Mhe. Ameir pia amehamasisha wazazi kushirikiana na shule kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya chakula shuleni kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016.



Maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni yalianzishwa mwaka 2016 kufuatia makubaliano ya Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, yakilenga kuhamasisha upatikanaji wa chakula na lishe bora kwa wanafunzi kupitia ushirikiano wa Serikali, mashirika ya kimataifa na jamii.