
Shule ya Msingi Ilboru, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, imenufaika na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa kupitia Mradi wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), unaotekelezwa na Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB).
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Philomena Mbiling’i, amesema ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo umegharimu Sh. milioni 112.6, ambapo madarasa matatu yanatumiwa na watoto wa Elimu ya Awali na moja linatumiwa na darasa la kwanza. Matundu sita kwa ajili ya wanafunzi wa Elimu ya Awali na walimu.
“Shule yetu ina jumla ya wanafunzi 1,629 kati yao wavulana 869 na wasichana 760, tulikabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa. Mradi wa BOOST, umeleta hamasa na chachu ya ujifunzaji kwa wanafunzi wakifurahi miundombinu safi" amesema Mbiling’i.
Mwalimu wa Elimu ya Awali katika Shule hiyo, Anna Marti, amesema anafundisha watoto 92 kati yao wavulana 50 na wasichana 42, wakiwamo wa mahitaji maalum kama vile wenye ulemavu wa ngozi na mmoja mwenye ulemavu wa viungo.
“Miundombinu mizuri imewafanya Watoto wetu kuelewa haraka, wanajifunza kwa vitendo kupitia hadithi, michezo na majadiliano. Pia wanapata elimu ya afya na lishe" amesema Marti.
Ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu umeongeza mahudhurio na ari ya watoto katika masomo yao, hayo ni mafanikio ya Mradi wa BOOST katika kuimarisha elimu ya awali na msingi nchini