Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya kwanza katika kata ya Makowo, shule ya Sekondari Makowo iliyojengwa kupitia Mradi wa kuendeleza Elimu ya Sekondari (SEQUIP)
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi Septemba 20, 2024 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewataka wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii na kuhimiza kupenda masomo ya sayansi na kueleza watakapomaliza kidato cha sita watakao faulu vizuri watanufaika na ufadhali wa masomo ya elimu ya juu kupitia Samia Scholarship
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita mbali ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na stashahada iliongeza ufadhili unaojulikana kama Samia Scholarship ambao unawalipia wanafunzi masomo kwa asilimia 100.
"Na hapa nataka mnielewe Samia Scholarship si mkopo, hivyo ukipata utawapunguzia wazazi mzigo na hela ya kusomesha, haya ni mafanikio makubwa katika sekta ya elimu." Amesema Mkenda
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Makowo Nikas Kampinga amesema kuwa shule hiyo imejengwa kwa gharama ya zaidi ya Milioni 583 ambayo imejenga madarasa, jengo la utawala na ofisi za walimu na kwamba serikali pia ilitoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga nyumba ya walimu yenye uwezo wa kuchukua familia mbili.
Aidha Mwalimu Mkuu huyo ameongeza kuwa wananchi wa Kata ya Makowo walichanga shilingi Milioni 27 na Halmashauri ya Mji Njombe ilichangia Shilingi Milioni 58 kutoka kwemye mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi bweni la wanafunzi
Shule ya Sekondari ya Makowo iliyo KM 85 kutoka Njombe Mjini yenye wanafunzi 92 wa kidato cha kwanza imepunguza sana umbali wa wanafunzi kutoka vijiji vitatu katika kata hiyo kufuata elimu ya sekondari.