
Serikali ya Tanzania inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu na kuongeza fursa mbalimbali zinazolenga kupata wahitimu mahiri katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya Taifa.
Hayo yamebainishwa Agosti 23, 2025 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf wakati akizungumza katika Shule ya Sekondari Emboreet iliyopo Wilaya ya Simanjiro, ambapo ametaja fursa hizo ikiwemo Samia Skolaship kwa fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi Elimu Tiba na Hisabati.
Ameongeza kuwa Serikali pia imeongeza fursa zaidi kwa kutoa ufadhili wa masomo katika ngazi ya Shahada ya kwanza na Shahada ya umahiri kupitia program ya Samia Scholarship Extended AI/DS inayolenga wanufaika fani za data science, artificial intelligence, cyber security, machine learning na allied sciences, watasoma katika Vyuo Vikuu bora Duniani.
"Nimeona miundombinu mizuri ya shule, nimetembelea maabara ya fizikia, biolojia na kemia. Wanafunzi wamenielezea vizuri, hii inadhihirisha mnajifunza kwa bidii na fursa za masomo elimu ya juu na ufadhili zipo wazi kwa ajili yenu" Alisema Waziri Mkenda.
Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Aziza Msengesi amesema Shule hiyo ya Serikali ilijengwa kwa ufadhili wa ECLAT Development Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Upendo la Ujerumani na inajivunia mafanikio mbalimbali ikiwemo ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi.
Kuhusu maombi ya usajili Shule hiyo kuwa ya bweni, Prof. Mkenda amemuagiza Mkuregenzi wa Halmashauri ya Simanjiro kuwasilisha maombi ya usajili Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na kwamba Wizara itafanyia kazi kikamilifu.