Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar Kipanga amesema serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Taasisi za Elimu ya Juu nyanja ya tehama ili kusaidia kuzalisha wataalam wengi na mahiri watakaosaidia maendeleo ya uchumi wa kidigitali.
Mhe. Kipanga ametoa kauli hiyo leo Novemba 17, 2023 jijini Arusha wakati akifungua Maadhimisho ya Miaka 6 ya Kituo cha Umahiri katika TEHAMA cha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM AIST), ambapo amesema ustawi wa baadaye wa uchumi wa Afrika utategemea kiwango cha uwekezaji katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi.
‘’Suala la ubunifu litaendelea kuwa muhimu katika ukuaji wa uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na usafirishaji, katika miongo ijayo uwezo wa uvumbuzi ni muhimu kwa ajili ya ushindani kitaifa na kimataifa’’ alisema Mhe. Kipanga
Aidha Mhe. Kipanga ameishukuru seriakali ya Ujerumani, kupitia Taasisi yake ya GIZ pamoja na DAAD kwa kufadhili mradi unaolenga kuwajengea uwezo wanafunzi wa eneo la Afrika Mashariki katika Masuala ya TEHAMA.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imewajibika kikamilifu katika kufanya uwekezaji mkubwa kwanza kwenye miundombinu, kusomesha wataalam mbalimbali lakini pia katika kuhakikisha inaandaa bajeti ambayo itawezesha masuala ya tehama kutumika kwa ufanisi.
‘’Katika Mwaka wa fedha 2023/24 serikali imetenga zaidi ya Bilioni 9 kwa ajili ya kuwezesha bunifu mbalimbali Pamoja na Teknolojia zilizoibuliwa ili ziende kuwa bidhaa zitakazosaidia kutatua changamoto zinazokabili jamii yetu’’ alibainisha Mhe. Kipanga.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Prof. Maulilio Kipanyula amesema tangu kuanzishwa kwa Kituo hicho wameweza kuzalisha wahitimu 136 ambao wanaotoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Prof. Kipanyula amesema kituo kinajivunia mafanikio makubwa ikiwemo kutoa ufadhili kwa Wanafunzi wote nchi za Afrika Mashariki kusoma katika Taasisi yao.