Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula leo Oktoba 11, 2023 amewahimiza Wananchi kutoka mikoa yote kutumia vema Maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu ya Watu Wazima, kuona mafanikio ya program mbalimbali za Kielimu zinazotplewa na Taadidi hiyo pamoja na Taasisi za Elimu ya Juu, Vyuo vya Kati na vya Ufundi.
Dkt. Rwezimula ametoa rai hiyo leo Oktoba 11, 2023 wakati akitembelea mabanda ya maonesho katika juma la Elimu ya Watu wazima linalofanyika katika Viwanja vya Maili Moja wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ili kujionea huduma zinazotolewa kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Juma hilo, Oktoba 13, 2023.
‘’nimefarijika kukuta Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo vingine ambavyo vinatoa mafunzo yanayohusu Elimu ya Watu Wazima wako hapa, lakini pia nimekutana na Vikundi vya Watu Wazima ambao wamenufaika na program mbalimbali zinazoendeshwa na Taasisi yetu ya Elimu ya Watu Wazima’’ alisema Dkt. Rwezimula.
Aidha Dkt. Rwezimula amefurahishwa kukutana na Vikundi vya Vijana wa Kike, ambao wamepewa fursa ya kurudi shuleni kupitoa Waraka wa Elimu namba 3 wa 2021 kuendelea na masomo, baada ya kukatiza kwa sababu mbalimbali.
‘’Mtakumbuka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alituelekeza Wizara ya Elimu, kuandaa mpango Maalum wa kuwarudisha vijana shuleni waweze kufaidika na fursa za masomo, na sasa vijana wengi wamerudi katika vituo mbalimbali’’. Alieleza Dkt. Rwezimula.
Naibu Katibu Mkuu huyo amevipongeza Vikundi vya Wanawake Watu Wazima ambao wamendelea kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa za kupata elimu bila kujali umri walionao, ikiwa ni pamoja na kuyatumia maarifa katika kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania.
‘’Nimefurahi kukutana na Vikundi vya wakinamama ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika, lakini kulingana na program ambazo zimeandaliwa wameweza kusoma lakini pia wameweza kuanzisha shughuli mbalimbali za kujipatia kipato’’. Alinena Dkt. Rwezimula.