Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amesema Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuharakisha ukuaji wa Uchumi katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, nishati na madini.
Dkt. Rwezimula amesema hayo Mei 13, 2023 jijini Arusha wakati akizindua Uanzishwaji wa Madawati na Majukwaa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, ambapo asema hatua hiyo itasaidia kuchagiza utafiti na Ubunifu unaofanywa kwa kuzingatia changamoto na mahitaji ya jamii.
"Madawati na Majukwaa haya yataimarisha mfumo wa uratibu na usimamizi wa shughuli za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika ngazi zote ikiwemo Serikali za Mitaa" alisema Rwezimula.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutenga fedha na rasilimali nyingine kwa ajili ya kuendeleza na kubiasharisha bunifu na teknolojia zinazoibuliwa kupitia Mashindano ya (MAKISATU) na njia nyingine.
Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Prof. Ladslaus Mnyone amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo Maafisa Elimu Kata na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Mikoa kuanzisha na kuendesha Madawati na Majukwaa yenye uwezo wa kuelimisha jamii, kuibua, kutambua na kuendeleza bunifu na teknolojia katika maeneo yao.
Akimwakilisha Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kaimu Mkurugenzi wa Elimu Msingi Mwl. Suzan Nusu amesema watasimamia na kufuatilia maelekezo yote kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya.
Afisa Elimu mkoa wa Arusha Bw. Abel Mtupwa ameipongeza Wizara hiyo kwa kuendelea kuwekeza katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na uboreshaji wa miundombinu katika sekta ya Elimu