Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inatoa mkopo kwa asilimia miamoja kwa Wanafunzi wanaofaulu zaidi masomo ya Sayansi kidato cha sita na kusomea nyanja za Sayansi, Elimu Tiba, Uhandisi, Hisabati na TEHAMA Elimu ya Juu



Mkenda amesema hayo Agosti 24, 2024 baada ya kuzindua Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi Dimbani na Dahalia ya Wanafunzi wa kike katika Skuli hiyo Kisiwani Unguja, akiwasisitiza Walimu kuwahimiza Wanafunzi kutumia fursa hiyo kikamilifu.



Waziri huyo ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kwenda sambamba na kasi ile ya uendelezaji wa elimu ambayo ndio mwelekeo wa Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.



"Katika mageuzi haya ya elimu tuliyoanzisha, tuna mambo mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar ya jinsi mnavyotekeleza. Tunahimiza elimu ujuzi na hapa tumetumia istilahi ya Amali ambayo hapa ndio inatumika" alibainisha Prof. Mkenda.