Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Ubunifu kitaifa yaliyofanyika katika Kiwanja cha Jamhuri Jijini Dodoma amesema maadhimisho ya Wiki ya Ubunufu ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) Mwaka 2019 wabunifu na wavumbuzi wachanga wapatao 2,636 waliibuliwa na kutambuliwa na Wizara.



“Wabunifu wengine 283 wanaendelezwa na Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili ubunifu wao ufikie hatua ya kuwa bidhaa na kuingia sokoni ili kuongeza fursa ya ajira na vipato kwa vijana wetu, wabunifu wachanga wanaendelezwa kwenye vituo atamizi na kumbi za ubunifu ambazo hadi sasa bunifu na teknolojia 53 zimefanikiwa kufikia hatua ya kuwa bidhaa na hivyo kutumika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo, maji , madini, afya, elimu,”amesema Prof. Nombo.

Amebainisha moja ya changamoto inayowakabili wabunifu wachanga ni kukosa mahali pa kuendeleza bunifu zao na kwa kutambua hilo serikali kupitia taasisi ya COSTECH imeanzisha kumbi za ubunifu na atamizi za DTB kwa lengo la kuendeleza vijana wenye mawazo ya ubunifu mbalimbali.

“Kuwepo wa kumbi hizi umechochea wadau Sekta za umma na bunifu kuanzisha kumbi za ubunifu na teknolojia zaidi ya 50 ili kuendeleza wabunifu wachanga, Serikali kupitia Buni Hub na DTB imewezesha kuanzishwa kwa kampuni changa mapya zaidi ya 94 na kutoa ajira na ajira zisizo za moja kwa moja kwa vijana zaidi ya 30,000 mchango wa kampuni hizo kwenye pato la Taifa ,”amesema Prof. Nombo.