Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amewataka wasimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa Mitambo ya Uchakataji maji taka, maabara na mitambo ya Biogas katika shule ya mfano Iyumbu kuongeza kasi ili kukamilisha kazi hizo.

Dkt. Rwezimula ametoa agizo hilo 31 Julai, 2023 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mifumo mbalimbali katika Shule mpya ya mfano iliyopo mkoani Dodoma, ambapo amewasisitiza Wahandisi kuongeza kasi zaidi ya ujenzi.

Akitoa maelezo kuhusu mfumo wa uchakataji maji taka Mhandisi wa Nishati Mbadala Irin Kimaro amesema utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuyachakata maji na kuweza kuyatumia katika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na upishi, umwagiliaji pamoja na kupata nishati ya Gas kwa ajili ya kupikia.

" Maji yanayotoka kwenye mtambo huo yatakuwa yametolewa aina zote za bacteria na virusi vinavoweza kusababisha maradhi hivyo tunaweza kuyatumia kwenye shughuli zingine za kila siku" alisema Kimaro.


Ujenzi wa Shule ya Mfano unatekelezwa na mradi wa Elimu wa kukuza ujuzi na uzalishaji wa ajira ( ESPJ ) chini ya Ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama zaidi ya shilingi billioni 17