Na WyEST
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejipambanua kuendelea kushirikiana na Vyombo vya habari katika kutangaza kazi inazofanya pamoja na matokeo ya utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na Wizara hiyo.
Akifungua mkutano na Wahariri wenye lengo la kuwajengea uelewa wahariri kuhusu Mradi wa Shule Bora uliofanyika jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Franklin Rwezimula amesema milango ya Wizara ipo wazi kupata taarifa ili kuendelea kuhabarisha umma.
Akizungumzia Mradi wa Shule Bora Dkt. Rwezimula amesema ni programu ya Serikali inayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID) kupitia Foreign, Commonwealth and Development Office (FCDO) kwa jumla ya Shilingi bilioni 271 (sawa na Paundi milioni 89) na itatekelezwa katika kipindi cha miaka 6, kuanzia mwaka 2021 hadi 2027.
“Ndugu wahariri katika Programu hii mikoa 9, Halmashauri 67 na zaidi ya Shule za Msingi na Awali 5,757 zitanufaika huku wanafunzi takribani milioni 3.8 na Walimu 54,000 watafikiwa katika utekelezaji wa programu hii. Tuendelee kutangaza mafanikio haya ili wananchi wayafahamu,” amesema Dkt. Rwezimula.
Dkt. Rwezimula ametaja mikoa itakayonufaika na Mradi kuwa ni Dodoma, Katavi, Kigoma, Mara, Pwani, Rukwa, Simiyu, Singida, na Tanga.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe amesema kufanyika kwa kikao hicho ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Mawasiliano wa Mradi na kwamba kazi hiyo ilianza katika ngazi ya mikoa na halmashauri ambapo mradi unatekelezwa ili kujenga uelewa wa mradi huo na kuweza kutangaza mradi na matokeo yake.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa hilo, Yasin Sadik amesema wako tayari kushirikiana na Wizara huku wakiiomba Wizara hiyo kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili taarifa za Sekta ya Elimu ziweze kuwafikia wananchi.