Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa ametoa wito kwa Wathibiti ubora wa shule na maafisa elimu kata kuwaheshimu walimu na kuwasikiliza ili kufahamu Changamoto zao hali itayosaidia kuboresha Sekta ya elimu nchini.

Dkt. Mtahabwa ametoa wito huo leo Desemba 30, 2023 Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya mtaala ulioboreshwa kwa wathibiti ubora wa shule na maafisa elimu kata, mtaala unaotarajia kuanza kutekelezwa kuanzia Januari 2024.

"Elimu katika nchi yoyote ile ni mwalimu, ukijua hilo jifunze kufanya kazi vizuri na mwalimu, jifunze kumheshimu mwalimu, kumpenda, kumthamini tusitoe maelekezo bila kuwapa elimu ya jambo lolote, naomba tutumie nafasi zetu vizuri na kuongea nao kwa staha." Amesema

Ameendelea kusema, Sera ya elimu ya 2014 toleo la 2023 inasisitiza kuinua hadhi ya elimu, hivyo ametoa wito kwa wataalamu hao kuwa wanyenyekevu kwa walimu wanaowaongoza na kuacha tabia ya ujuaji wa kila kitu, hali itayosaidia kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Elimu nchini.



Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Msingi na Elimu ya Awali kutoka OR TAMISEMI Bi Suzanne Nusu amesema, kama watekelezaji wa Sera katika ngazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa watahakikisha wanatoa ushirikiano kwa Wizara ya Elimu na Taasisi ya Elimu ili Mtaala huu ulioboreshwa unaenda kuwa chachu ya mabadiliko katika Sekta ya Elimu.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba ametoa wito kwa wathibiti ubora wa shule kuzingatia kwa undani mafunzo haya yanayotolewa na TET ili kwenda kuwafundisha walimu wote kwenye kata zao kuuelewa mtaala mpya na namna bora ya kuutekeleza.



Amesema, Maafisa elimu kata na Wathibiti ubora wa shule ni wawakilishi wa TET katika maeneo yao ya utendaji hivyo ni muhimu kusaidia kutatua changamoto zinazowakumba walimu katika shule zao badala ya kuandika taarifa ya changamoto hizo bila kusaidia utatuzi.

Dkt. Komba amesema, Taasisi ya Elimu Tanzania itaendelea kushirikiana na Maafisa Elimu Kata pamoja na Wathibiti ubora wa shule ili kuhakikisha ubora wa elimu unatekelezwa katika ngazi zote ikiwemo kupitia mitaala iliyoboreshwa.