Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arumeru Bw. Kennedy Mpumilwa ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uwekezaji wa miundombinu ya elimu Shule ya Sekondari Patandi Maalum na Chuo cha Ualimu Patandi jijini Arusha.



Bw. Mpumilwa ametoa pongezi hizo Septemba 19, 2024 akizungumza alipotembelea maonesho katika maadhimisho ya Miaka 30 ya Elimu Jumuishi.



"Tunampongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uwekezaji wa miundombinu mbalimbali katika Shule ya Sekondari Patandi na Chuo cha Ualimu Patandi. Miundombinu hii inahamasisha ujifunzaji kwa wenye mahitaji maalum hivyo kutoa fursa kwa watoto wote kupata elimu" alisema Bw. Mpumilwa.



Ameongeza kuwa uwepo wa Shule Jumuishi Nchini unaongeza ari kwa jamii kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Sera ya Elimu.



Bw. Mpumilwa ameambatana na Viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi kutoka Wilaya ya mjini Visiwani Zanzibar kushuhudia utekelezaji wa miradi ikiwemo miradi ya Elimu katika Mkoa huo.