
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema Serikali kupitia wizara hiyo inaendelea kusimamia kwa karibu mapitio ya muundo na mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa lengo la kuboresha mifumo ya upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Prof. Mushi ameyasema hayo leo tarehe 28 Januari 2026 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa huduma mpya kwa wateja inayotumia Akili Unde (AI) maarufu kama ‘BWANABOOM’, itakayowezesha upatikanaji wa taarifa na huduma za HESLB kwa urahisi zaidi.

Amesema mapitio ya mifumo hiyo yanalenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa mikopo, kuhakikisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati, kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchakato wa upangaji na utoaji wa mikopo, pamoja na kupunguza adha ya wanafunzi na wanufaika kusafiri umbali mrefu au kusubiri kwa muda mrefu ili kupata huduma.

Prof. Mushi ametoa wito kwa wanafunzi, wanufaika wa mikopo, wazazi, walezi, wadau wa elimu na Watanzania kwa ujumla kuitumia huduma ya ‘BWANABOOM’ ili kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema ubunifu wa BWANABOOM ni sehemu ya safari ya kimkakati wa taasisi hiyo anayoiongoza katika kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa, kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa upatikanaji wa taarifa.


