Serikali imesema utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na Mitaala mipya kwa elimu ya Sekondari itaanza mwakani kwa mkondo wa elimu ya Amali.

Akizungumza Disemba 18, 2023 Jijini Dar ea Salaam wakati akiongea na Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yatatekelezwa kwa awamu ambapo madarasa yatakayoanza na mitaala mipya ni awali, la kwanza na la tatu kwa shule za msingi na kidato cha kwanza shule za mkondo wa Amali pekee.

Kiongozi huyo amesema mkondo wa elimu ya amali utakuwa na masomo ya taaluma kidogo na una machaguo 60 ya programu za stadi ambazo mitaala imeandaliwa na VETA na kutolewa ithibati na Baraza la Taifa la Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na kwamba mwanafunzi anapomaliza kidato cha nne anapata vyeti viwili ambavyo ni cha sekomdari na ufundi (Amali).

Waziri huyo ameongeza kuwa ili kuruhusu shule kutoa mafunzo ya amali tutafanya tathmini ili kuhakikisha mambo yote muhimu yamekamilika ikiwemo kuwa na karakana, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na walimu ili kuwezesha wanafunzi kupata elimu inayotakiwa.



Ameongeza kuwa kwa mwaka 2024 shule zilizokuwa za Ufundi na Kilimo anbazo zina karana na vifaa vya kufundishia na kujifunzia zitaanza kutumia mkondo wa elimu ya amali.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa mageuzi ya elimu yaliyofanyika nchini yalikuwa yanahitajika na kila mtu nchini na kwamba Duniani kote pia kuna michakato mbalimbali inaendelea ya mageuzi katika elimu ambayo yanalenga kuwapatia vijana stadi za ujuzi utakaowawezesha kuingia katika soko la ajira bila changamoto zozote.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa nwa Dar es Salaam Khadija Said amesema kuwa Jumuiya hiyo inajivunia namna serikali ilivyofanya mageuzi makubwa ya elimu nchini ambayo yanakwenda kuwafanya vijana wa kitanzania kuwa na umahiri kwa kuwapatia stadi na maarifa yatakayowawezesha kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa.



Ameongeza kuwa Jumuiya hiyo ambayo inamiliki shule nchini ni mdau mkubwa wa elimu na kwamba ilishiriki katika makangamano na mikutano ya kujadili mageuzi hayo.