Mfumo wa tathmini endelevu umetajwa kuwa chachu ya kubadilisha mwelekeo wa elimu msingi nchini, kwa kuweka mkazo katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa karibu na kuboresha ubora wa ufundishaji.



Akizungumza Aprili 16, 2026 jijini Dodoma, katika kikao cha wadau wa elimu cha kujadili taarifa ya tathmini ya ujifunzaji wa elimu msingi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Prof. Said Mohamed, amesema tathmini endelevu inawasaidia walimu kufuatilia hatua za ujifunzaji darasani na kubaini mapema changamoto kabla ya mitihani ya mwisho.



Aidha amesisitiza kuwa Baraza linaendelea kuimarisha mifumo ya upimaji ili matokeo ya tathmini yaendane na uhalisia wa ujifunzaji na kusaidia kuboresha ujuzi wa wanafunzi.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu Msingi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Abdul Maulid, amesema Serikali imeweka mkazo katika kufanya tathmini endelevu ili kuimarisha ubora wa ufundishaji shuleni.



Ameongeza kuwa mfumo huo utasaidia kuongeza uelewa wa wanafunzi na kupunguza changamoto ya kupanda madarasa bila umahiri wa kutosha, huku mafunzo kwa walimu yakiendelea kuboreshwa ili kuongeza ufanisi.