Maafisa Habari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi zinazotekeleza Mradi wa EASTRIP (East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project)

wamekutana jijini Dar es Salaam kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha mradi unatangazwa na jamii inaufahamu.



Kikao kazi hicho kimeanza Septemba 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT ambapo Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ambaye pia ni Mratibu wa Mradi huo Fredrick Salukele ameelezea namna mradi huo wa miaka mitano ulivyotekelezwa kwa mafanikio mpaka sasa.



Mkurugenzi huyo amesema kuwa Mradi wa EASTRIP unatekelezwa katika nchi tatu ambazo ni Kenya, Ethiopia na Tanzania na unajenga vituo vya umahiri katika fani mbalimbali.



Ameongeza kuwa hapa nchini mradi huo unatekelezwa katika Chuo cha Ufundi Arusha wanaojenga kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu, Taasisi ya Dar es Salaam ya Teknolojia DIT kampasi ya Mwanza ambao wanajenga kituo cha Umahiri wa mazao ya ngozi, ambapo DIT Dar es Salaam wanajenga Kituo cha Umahiri cha TEHAMA na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT kinajenga Kituo cha Umahiri cha Usafirishaji wa Anga.