Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewataka Wanataaluma kutafiti na kujadili historia ya nchi kwa uwazi na uzalendo ili kuhakikisha haipotoshwi hivyo kusaidia vizazi vijavyo kuwa na taarifa sahihi ajili ya maendeleo.
Prof. Mkenda ametoa rai hiyo Januari 06, 2024 Visiwani Zanzibar wakati akifungua Kongamano la Kitaaluma la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), ambapo amesema Wanataaluma wanapaswa kushiriki katika kuenzi Mapinduzi hayo ili kujenga jamii yenye ustawi wa kisiasa na hata kiuchumi.
"Vyuo Vikuu vina jukumu la kuchambua historia ya nchi yetu kwa uwazi na uzalendo ili kuhakikisha inatunzwa na kwamba haipotoshwi ili vizazi vinavyokuja vielewe mazuri yaliyofanyika na jinsi yalichochea uchumi ambayo ni tafsiri sahihi ya kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu inayosema 'Tuimarishe Uchumi, Uzalendo na Amani kwa Maendeleo ya Taifa letu" alisema Prof. Mkenda.
Aidha amesisiza jamii kuzingatia na kuikumbuka kikamilifu dhana ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964, inayosisitiza binadamu wote ni sawa bila kujali hali zao.
"Zanzibar ni sehemu ya Muungano wa Tanzania, leo hii ndani ya nchi yetu tunajivunia tunaye Rais Mwanamke, tunampongeza sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuenzi tunu zetu na kutuletea Maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Uchumi, Elimu, Afya na miundombinu mingine" alibainisha Waziri Mkenda.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Prof. Mohamed Makame ameeleza kuwa kinaendelea kuthamini kuheshimu na kuenzi mambo yote yaliyoasisiwa kwasabsbu yameleta mafanikio makubwa ikiwepo kuwezesha kuwa na Uhuru, Umoja na mshikamano wa dhati.
Ameongeza kuwa SUZA inaendelea kuleta mageuzi katika kutoa Taaluma kuanzia ngazi ya Stashahada hadi shahada ya Uzamivu, kufanya tafiti pamoja na kutoa ushauri wa kitaaluma kwa Wadau mbalimbali.
Nae Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed amesema Kongamano hilo litasaidia kutoa uelewa kwa vijana hasa Wanafunzi na kutathimini maendeleo ya Elimu na uchumi.