Tanzania inajivunia kutekeleza kwa vitendo hatua za kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki katika ngazi zote za elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amesema hayo Oktoba 11, 2023 jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yaliyojikita kusherehekea mafanikio ya mtoto wa kike kwenye elimu na kufanyika jijini Dodoma
Ametaja baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania inajivunia kwenye elimu kuwa ni pamoja na mpango wa kuwarejesha shule wanafunzi waliokatisha masomo wakiwemo wasichana.
Ameongeza kuwa kupitia mpango huo wanafunzi wa kike 7,995 wamerejea shule kupitia mfumo rasmi na usio rasmi kupata elimu ili kutimiza ndoto zao.
Prof. Mkenda amesema juhudi mbalimbali zilizofanyika Tanzania ni pamoja na kupitia Sera, Sheria na Nyaraka mbalimbali ili kuhakikisha watoto wote akiwemo wa kike anapata fursa sawa ya elimu. Ametaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni kutungwa kwa sheria ya Haki za Mtoto ya mwaka 2009 na kutoa Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2021 kuhusu urejeshwaji wa wanafunzi waliokatisha masomo katika elimu ya sekondari na msingi.
“Nina salamu zangu kwa UNICEF naialika ishirikiane na wizara yetu ya elimu kufanya utafiti kwa kufuatilia wale wote ambao wamerudi shule mmoja mmoja kumhoji kuangalia mazingira, mafanikio, changamoto na kuja na mapendekezo ya namna bora zaidi ya kutekeleza maelekezo haya ya Rais Samia ya kuhakikisha hakuna mtoto atakayeachwa nyuma kwenye elimu,”amesema Prof. Mkenda.
Aidha, amesema wanafunzi wa kike wananufaika na mikopo na kwa Mwaka 2022/23 serikali ilianza mpango wa Samia Scholarship kwa wanafunzi waliofaulu vizuri kwenye masomo ya sayansi kidato. Kati ya wanfunzi 636 walionufaikawanafunzi wa kike 261 sawa na asilimia 41.
“Kumekuwapo na mazingira wezeshi kupitia miongozo, miundombinu na vifaa mbalimbali yaliwezesha watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu, kila mwaka serikali inatenga fedha ya kununua vifaa,”amesema Prof Mkenda