Na WyEST Dar es Salaam
Serikali imesema maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mitaala imezingatia umuhimu wa Somo la Elimu ya Dini
Haya yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Disemba 05, 2024 wakati akikabidhi Vitabu vya Somo la Elimu ya Dini kwa Mufti na Shelkh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zuberi Bin Said Ally na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Al - Ka'ab ambapo amesema kuwa Mafunzo ya Somo la Elimu ya Dini kwa Dini zote ni lazima kuanzia Darasa la Kwanza mpaka Kidato cha Sita.
Waziri huyo amebainisha kuwa Mafunzo hayo katika shule yatatolewa na viongozi wa dini inayohusika kwa kuzingatia Mwongozo uliotolewa na Kamishna wa Elimu katika Waraka Na 5 wa Mwaka 1998
Ameongeza kuwa mbali ya Somo la Elimu ya Dini kuna masomo ya Bible Knowledge, Divinity na Somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu na kwamba Mtaala umebainisha umuhimu na lengo la kufundisha somo hilo.
Prof. Mkenda ametaja umuhimu na lengo hilo kuwa ni pamoja na kukuza maadili, na tabia njema, kuwezesha wanafunzi kuelewa na kuthamini wengine, kukuza mshikamano katika jamii.
Mufti na Shelkh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakari Zuberi Bin Said Ally ameshukuru na kuipongeza Serikali kwani imekuwa ikitekelza mambo mbalimbali waliyokubaliana kati yake na BAKWATA na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar wenye jukumu la kusimamia chombo kinachoandaa Mihutasari na Machapisho mbalimbali ya Masomo hayo.
Vitabu vilivyokabidhiwa ni 3000 vina thamani ya shilingi Milioni 32 na vimechapishwa na Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).