
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza rasmi uzinduzi wa Tuzo ya Uandishi Bunifu kwa Kiswahili, akitoa wito kwa waandishi kuwasilisha miswada yao kwa Kamati ya Kitaifa ya Tuzo.
Prof.Mkenda ametangaza uzinduzi huo Agosti 6, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa waandishi wa habari baada ya kikao cha awali na wadau wa uandishi bunifu kujadili maboresho ya tuzo hizo.
Aidha, Waziri huyo amewataka Waandishi bunifu kutumia fursa hiyo kuonyesha ubunifu na kuendeleza matumizi ya Kiswahili kupitia kazi zao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, ameeleza kuwa miswada itakayoshindanishwa itahusu Riwaya, Ushairi, Hadithi za Watoto na Ushairi wa Kiswahili. Kupokelewa kwa miswada kutaanza
Agosti 15 hadi Novemba 30, 2025. Ametoa rai kwa waandishi wa rika na mikoa yote kujitokeza kwa wingi.
Hafla ya kutangaza washindi itafanyika Aprili 13, 2026, kama sehemu ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amewashukuru wadau waliochangia maboresho ya tuzo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza usomaji, uandishi na ukuzaji wa Kiswahili nchini