#Benki hiyo kuendelea kushirikiana na serikali kutekeleza mageuzi ya elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Novemba 12, 2024 akiwa jijini Kigali nchini Rwanda amekutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi Victoria Kwakwa, pamoja na mambo mengine Mkenda ameishukuru Benki hiyo kwa namna inavyoshirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa ujumla wake.



Prof. Mkenda amemweleza Bi. Kwakwa kuwa Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya Elimu na sasa imeanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023.

Aidha Waziri Mkenda ameiomba Benki ya Dunia kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa mageuzi hayo hususan katika maeneo ya miundombinu, vitabu na upatikanaji wa walimu ili kufanikisha utekelezaji wa Sera ya elimu na mafunzo ya 2014 toleo la 2023.



Bi. Kwakwa ameipongeza Serikali, kutekeleza kwa vitendo mageuzi ya elimu ambayo yameifanya Tanzania kuwa kinara barani Afrika na kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi zinazopambana na maboreho ya elimu.

Amesema kuwa nchi nyingi zinatamani kusikiliza na kupata uzoefu wa Tanzania namna inavyotekekeza mageuzi ya elimu na miradi mbalimbali, hivyo ameipongeza kwa namna inavyoshirikiana na Benki hiyo katika kutekeleza kwa ufanisi hususan mradi wa SEQUIP, BOOST na ESPJ.



Amemhakikishia Waziri Mkenda kuwa atafanya kila linalowezekana kuona namna ya kuunga mkono maeneo hayo katika kutekeleza Sera hiyo.

Prof. Mkenda ameshiriki mkutano wa Elimu "Africa Foundation Learning Exchange" ulifanyika nchini humo, ambapo ametumia Mkutano huo kuwasilisha mageuzi ya elimu yanayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara.

Katika Mkutano huo ameambatana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia DKt. Charles Mahera, Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa pamoja na Viongozi mbalimbali