Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga amewahimiza wasimamizi wa mradi wa Ujenzi wa VETA ya Wilaya ya Arumeru kukamilisha hatua ya kwanza ya kujenga Msingi kwa wakati na kuwataka kufanya marekebisho katika maeneo yenye Changamoto zilizobainika.
Mhe. Kipanga ametoa rai hiyo Desemba 19, 2023, akiwa katika ziara ya Kukagua na kufanya tathmini ya ujenzi wa VETA hiyo ikiwa ni moja ya VETA 63 zinazojengwa na Serikali nchini.
Katika hatua ingine Naibu Waziri kipanga amewataka mhandisi na mshauri elekezi kuwepo eneo la ujenzi wakati wote ili kuhakikisha mafundi wanajenga kwa ufanisi na kufuata taratibu zote za ujenzi.
Aidha amehimiza umakini kwa mafundi wanaojenga karakana na madarasa ya chuo hicho kufuata maelekezo yote wanayopewa na wahandisi sambamba na vipimo na michoro iliyopo kwenye ramani za ujenzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru Jeremia Kashiri ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha za Ujenzi wa chuo hicho cha wilaya na kumshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ukaguzi, tathmini na kushauri.