Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema serikali inatambua mchango wa Wanahabari unaosaidia kutangaza teknolojia zinazochangia katika mabadiliko endelevu ya Kilimo Barani Afrika.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Disemba 2, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye halfa ya Tuzo za Uandishi wa Habari za Sayansi na Teknolojia upande wa Kilimo yaani _OMAS Media Awards
"Kupitia mawasiliano yenye ufanisi na Uandishi unaowajibika Bioteknolojia ina uwezo wa kuleta mapinduzi katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, pamoja na kuboresha maisha ya jamii zetu" Alieleza Prof. Mkenda.
Waziri huyo ameongeza kuwa katika ulimwengu wa sasa, ambapo taarifa zimekuwa nyingi jukumu la waandishi wa habari linazidi kuwa muhimu zaidi kwa Mataifa yanayoendelea, kutokana na kazi kubwa wanayofanya ya kuchambua kwa kina taarifa mbalimbali, inasaidia jamii kuwa na mitazamo chanya na kushawishi mijadala ya sera, na hata kuchangia katika kufanya maamuzi sahihi.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt. Amos Nungu amesema Tuzo hizo zinalenga kuhamasisha Uandishi wa habari za Kisayansi kwa upande wa kilimo ili kuisaidia jamii kupata tafsiri kwa urahisi na kufahamu maudhui yanayokusudiwa ili kuongeza uzalishaji wenye tija.
Ameongeza kuwa tuzo hizo zinaandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Open Forum on Agricultural Biotechnology in Africa (OFAM), Taasisi ya African Agricultural Technology Foundation (AATF) pamoja na COSTECH.