Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Bw. Ephraim Simbeye amesema jumla ya Walimu Wakuu 8,851 watapatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo kuhusu uongozi na usimamizi fanisi wa shule wanazosimamia.
Bw. Simbeye amesema hayo Septemba 22, 2024 jijini Mwanza akimwakilisha Katibu Mkuu Prof. Carolyne Nombo kufungua mafunzo kwa Walimu Wakuu awamu ya tatu kutoka mikoa 13 Tanzania Bara, ambapo amesema mafunzo hayo yanaendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), chini ya Mradi wa Kuimarisha Shule za Awali na Msingi (BOOST).
Amesema awamu ya kwanza ya mafunzo hayo yalihusisha walimu wakuu 4,522 katika Mikoa 7 na awamu ya pili yalihusisha Walimu Wakuu 4,620 katika Mikoa 6 ya Tanzania Bara.
Mkurugenzi huyo amewataka Walimu Wakuu kuhakikisha wanazingatia mafunzo na kwenda kuyatekeleza kwa vitendo hasa maeneo ya usimamizi wa ujenzi wa miundombinu, utunzaji wa kumbukumbu, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji na utunzaji wa takwimu za elimu shuleni.