
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Watu Wazima, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Mwalimu Ernest Hinju amesema kuwa uwajibikaji, uadilifu na uzalendo ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.
Mwalimu Hinju amesema hayo Septemba 16, 2025 mkoani Katavi akiwasilisha mada kuhusu Muundo wa Uongozi bora kwenye Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.
“Katika utawala bora wa elimu kiongozi anapaswa kuwa na sifa stahiki za kitaalam na kitaaluma, mtumiaji mzuri wa lugha katika mawasiliano na mfuatiliaji wa shughuli za kielimu mpaka mafanikio yapatikane" alisisitiza Kiongozi huyo.
Kwa upande wake Mshauri Mafunzo kutoka Shirika la Kimataifa DVV Bw. Mateo Mwita ameeleza kuwa katika kuipa msukumo elimu ya Watu Wazima, Shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali inaendelea kujenga mifumo endelevu ikiwemo Kuanzisha Vituo vya Jamii vya Kujifunzia (CLC).
Amesema vituo hivyo vinatoa fursa ya ujifunzaji na elimu endelevu ya Watu Wazima ili kuboresha stadi mbalimbali kwa jamii.
Naye, Afisa Elimu Wilaya ya Kibaha Meckitilda Kahindi amesema wanajivunia mafanikio makubwa ya kutokana na vituo hivyo ikiwemo kuwa na mashamba darasa yanayowezesha wanakisomo kujifunza mbinu bora za kilimo, ufugaji na ujasiriamali.