Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayesimamia Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa Afrika Mashariki kuhusu ujumuishi katika Elimu ya Juu kikanda unaofanyika tarehe 9 hadi 11 Septemba 2025 jijini Kampala, Uganda.



Mkutano huo umefunguliwa rasmi leo na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ukiwa na lengo la kuthibitisha dhamira ya kisiasa, na kuharakisha utekelezaji wa mifumo ya kikanda ya kuimarisha ulinganifu, uthibiti ubora, na utambuzi wa sifa za kielimu Afrika Mashariki.



Mkutano huo umeandaliwa na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Urekebu kwa kushirikiana na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), ambapo pia unalenga kutathmini hatua zilizofikiwa katika kuwezesha uhamaji wa wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na kuimarisha ujuzi na vipaji.