Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewataka Wakufunzi katika Chuo cha Ualimu tarajali Korogwe jijini Tanga kufahamu mwelekeo wa elimu, na kuhakikisha wanawajibika kikamilifu katika kutekeleza mabadiliko ya Elimu yanayolenga kuimarisha ufundishaji kidijitali.
Nombo ametoa rai hiyo Mei 29, 1024 jijini Tanga wakati akizungumza na Wakufunzi na Wafanyakazi Mwega wa Chuo hicho kuhusu masuala mbalimbali ya Elimu.
"Tumeanza kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, naomba tushirikiane kutekeleza mabadiliko hayo tukumbuke hatufundishi Vijana ili waajiriwe Tanzania pekee, tunataka wakaajiriwe Mataifa mbalimbali, lakini tuhakikishe tunatoa Wahitimu mahiri na Kwa kuzingatia viwango bora" alisema Prof. Nombo
Aidha amesema Serikali ina mpango wa kuboresha nyumba za Wakufunzi hatua kwa hatua ili kuboresha mazingira na kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Mkuu wa Chuo cha Ualimu Korogwe Hassan Ismail ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kukipatia vifaa vya TEHAMA na vifaa vya maabara na kemikali na kwamba vimewezesha ufundishaji na Ujifunzaji.