Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bushungwa, amesema Vijana wana nafasi kubwa ya kushiriki katika kukuza Uchumi na kudumisha amani iwapo watalelea na kukuzwa katika Maadili mema.



Ameyasema hayo, Disemba 14, 2024, Jijini Dodoma, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Dotto Biteko, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania ambapo amesema kulea vijana ni jukumu la kila mmoja na kwa kufanya hivyo itawezesha nchi kuwa taifa lenye vijana wwnye maadili shupavu na jamii imara yenye ustawi mzuri.



"Natambua kanuni yenu isemayo Skauti ni usafi wa mawazo, maneno, na matendo. Hivyo, nitoe rai kwa skauti wote nchini kuwahimiza vijana wengine ambao si Skauti kuwa waadilifu, waaminifu, na wenye kumcha Mungu."



Sambamba na hilo, amewataka skauti wote nchini kufanya matendo mema na kuachana na matendo maovu yanayoharibu mila, desturi, tamaduni, na maadili yetu, kwa dhumuni la kujenga taifa safi na imara lisiloyumbishwa na tamaduni za kigeni zisizo faa.



Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Skauti Tanzania, Profesa Adolf Mkenda, amesema Skauti inasaidia katika kukuza na kulinda maadili, kuendeleza ujasiri kwa vijana, na kuwasaidia vijana kujishughulisha na shughuli zenye maendeleo kwa nchi yetu.



"Wizara ya Elimu kupitia waraka wa Elimu Namba 4 wa mwaka 2015 unahimiza kukuza Skauti katika ngazi zote za elimu, na sisi kama wizara tumejipanga ipasavyo kukuza shughuli mbalimbali za skauti katika jamii. Tunawahasa wengine kutuunga mkono katika kutekeleza hilo," alisema Profesa Mkenda.