Naibu Katibu Mkuu Elimu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Charles Mahera amesema Serikali katika Mwaka 2023/2024 na 2024/2025 imetoa takribani Shilingi bilioni 6 kwa ajili ya mafunzo endelevu kazini kwa walimu kazini wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa nia ya kuongeza ujuzi na umahiri kwa Walimu wa masomo hayo.
Ameyasema hayo Novemba 7 2024, Mkoani Morogoro wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya mafunzo endelevu ya Walimu kazini wa masomo ya Hisabati na Sayansi (Kemia, Fizikia na Biolojia)
Dkt Mahera amesema uwekezaji katika mafunzo hayo unaendana na utekelezaji wa sera ya Elimu ya kuhakikisha walimu na wataalamu katika elimu wanapata mafunzo endelevu kazini.
"Masomo ya Sayansi hufanya watu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kuja na masuluhuhisho ya changamoto mbalimbali na pia suluhu zinazowezesha kuchangia Maendeleo ya kijamii na Kiuchumi kwenye nchi yetu" alisema
Ameongeza "Tuendelee kuwekeza nguvu nyingi kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye masomo yote ya Sayansi kwa sababu kwenye mtaala wa nyuma tulijikita sana kwenye nadharia zaidi kuliko vitendo" alisema dkt mahera