
Mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa elimu ya watu wazima, wakiwemo maafisa wa magereza, yamezinduliwa rasmi leo jijini Dodoma, Mafunzo hayo yanaendeshwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), yakiwa na lengo la kukuza ujuzi na stadi bunifu kupitia mbinu mpya ya RIFLEKTI inayolenga kuimarisha maarifa ya msingi ya KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) pamoja na stadi za maisha.
Akizindua mafunzo hayo hii leo Julai, 28, 2025 Jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu WyEST, Dkt. Hussein Omar, alisisitiza umuhimu wa elimu ya watu wazima kama silaha dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi, huku akiipongeza TEWW kwa juhudi zake za kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wote, wakiwemo waliopo katika vituo vya urekebishaji wa tabia.
Dkt. Omar ametaja mafanikio ya programu bunifu kama MUKEJA, MECHAVI (IPOSA) na sekondari mbadala, akisema zimechangia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha vijana waliokatika mfumo rasmi wa elimu kurejea kwenye mkondo sahihi wa maendeleo binafsi na ya taifa.
Naye Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Philipo L. Sanga amesema kuwa TEWW ipo katika mchakato wa kufanya elimu ya watu wazima kuwa ya kisasa zaidi, ikiwemo kuwafikia walengwa walioko magerezani kwa kutoa elimu ya marekebisho itakayowawezesha kujenga maisha mapya baada ya vifungo.
Mafunzo haya yanatolewa wakati ambao TEWW inaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Washiriki wa mafunzo wanatarajiwa kuwa viongozi wa mabadiliko ya kijamii, watakaotumia maarifa na ujuzi wanaopata kuimarisha uzalishaji, kukuza ujasiriamali na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii zao