
Serikali ya Tanzania kupitia Mradi wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) inatekeleza Mpango wa Shule Salama ili kuimarisha mazingira ya ujifunzaji shuleni na kutoa fursa ya elimu bora, salama na jumuishi kwa kila mtoto bila ubaguzi.
Katika Shule ya Msingi Nasholi, Halmashauri ya Meru mkoani Arusha, mpango huu umewezesha wanafunzi kujitambua na kuonesha uwezo wao bila hofu. Wameimarika katika stadi za maisha na umewawezesha kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia, hali iliyochangia kukuza hali ya usalama na kujiamini.
Niwael Mbise, Mwanafunzi na Mwenyekiti wa Baraza la la Kupinga Ukatili wa Kijinsia shuleni hapo, amesema mpango huo umewajengea uwezo wa kutambua aina za ukatili wa kijinsia na mbinu za kukabiliana nazo, hatua iliyoboreshwa ustawi wao shuleni na hata nyumbani.
Mwalimu wa Unasihi wa Shule hiyo, Anambora Swai, amesema Mpango wa Shule Salama umeleta mafanikio katika kuimarisha mahusiano baina ya walimu, wazazi na wanafunzi na kwamba umechangia kuongezeka kwa ushiriki wa wanafunzi darasani na kuboresha mazingira ya kujifunza.
Jumla ya shule 3,800 kati ya 6,000 zinazolengwa nchini tayari zimeanza kutekeleza mpango huo, ambapo walimu wanasihi 3,800, walimu wakuu 3,800 pamoja na waratibu elimu kata 680 wamepatiwa mafunzo ya kujengewa uwezo ili kutekeleza kwa ufanisi.