Na WyEST
Dar es Salaam

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 imepanga kuongeza nyanja za ushindani katika kuwania Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo Oktoba 24, 2023 Jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika uzinduzi wa Kitabu cha Mwandishi Abdulrazak Gurnah kilichotafsiriwa katika lugha ya kiswahili kijulikanacho kwa jina la Peponi.

Prof. Nombo amesema kuwa kuongezeka kwa nyanja mbalimbali ikiwemo vitabu vya watoto vilivyoandikwa katika mazingira ya kitanzania kutasaidia kuwa na vitabu vinavyozingatia mila, desturi na tamaduni za Mtanzania.



"Tunaamini kuwa kuongezeka kwa wigo wa nyanja mbalimbali itaongeza ushindani wa washiriki lakini pia itahamasisha uandishi na kuwa chachu ya kuibua vipaji vingi vya waandishi bunifu na kuleta mwamko wa usomaji wa vitabu vilivyoandikwa na kutafsiriwa katika lugha ya taifa ya kiswahili" anesema Prof. Nombo

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Serikali imejipanga kununua vitabu muhimu kama vya viongozi na vilivyoandikwa na watanzania ili kuvisambaza katika maktaba ya Taifa, Mikoa na Shule ili kuongeza ari ya utamaduni wa kujisomea na kupata maarifa.



Akizungumza katika uzinduzi huo Mwenyekiti wa Kampuni ya Uchapishaji ya Mkuki na Nyota Walter Bgoya amesema watanzania wanapaswa kujivunia kitabu hicho ambacho kilishinda tuzo ya nobeli kwa kuwa kimeandikwa na mtanzania na kwamba kutafsiriwa katika lugha ya kiswahili ni jambo muhimu kwa kuwa kinatoa fursa kwa watanzania kuweza kukisoma na kukielewa



Naye mchapishaji wa kitabu hicho kilichotafsiriwa katika lugha ya Kiswahili, Mkuki Bgoya ameiomba serikali kuhamasisha uandishi na usomaji wa vitabu kwa kununua vitabu vinavyoandikwa na kuchapishwa na watanzania kwa ajili ya kuvisambaza katika maktaba za wilaya, mikoa na shule.