WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili imetumia shilingi trilioni 1.29 kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 454.3 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya awali na msingi ambapo jumla ya shule mpya zilizojengwa ni 342, vyumba vya madarasa 9,189, nyumba za walimu 346, mabweni 28 na ukarabati wa shule kongwe 45.
Amesema hayo leo (Alhamisi, Februari Mosi, 2024) Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Amesema utekelezaji wa mtaala mpya umeanza katika ngazi ya Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi - Darasa la I na III, Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza katika baadhi ya fani za amali katika shule 96 za Serikali na Binafsi ambazo zina miundombinu wezeshi kama karakana na Walimu wa fani hizo.