Mwandishi nguli wa vitabu, Mwl. Abdilatif Abdalla, amesema uandishi bunifu haupaswi kuchukuliwa kama anasa, bali ni nyenzo muhimu ya kujenga fikra, kuelewa jamii na kuibadilisha.



Akizungumza kama mgeni rasmi katika usiku wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Mwl. Abdalla alisisitiza kuwa ubunifu wa lugha iwe maandishi au masimuliziuna jukumu kubwa la kuelimisha, kuibua tafakuri na kuchochea maendeleo ya kijamii.



Kwa mujibu wake, mshairi ana nafasi ya kipekee katika jamii kwa kuwa mara nyingi huwa mbele ya wakati wake, akiona na kutabiri mambo kabla hayajatokea. Alieleza kuwa ushairi hauishii kueleza hisia pekee, bali huchambua, huhoji na kuwasilisha ukweli wa maisha kwa kina.



Mwl. Abdalla alifafanua zaidi kwamba dhana ya ushahidi katika ushairi inahusisha uwezo wa mshairi kujua, kuelewa na kuchambua hali halisi ya jamii, na kubuni taswira zinazoweza kuathiri fikra na mwelekeo wa jamii yenyewe.



Aidha, alisisitiza kuwa uhai wa jamii yoyote unategemea utamaduni wa kusoma na kuandika, akihimiza kuendelezwa kwa machapisho na kazi bunifu ili kuimarisha maarifa na fikra za wananchi.



Mwl. Abdalla aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha tuzo hizo miaka minne iliyopita, akieleza kuwa ni hatua muhimu ya kukuza na kuthamini uandishi bunifu nchini.