Na Mwandishi wetu 

Wananchi wa Kijiji cha Chiponda, Kata ya Chiponda Tarafa ya Rondo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi wamenufaika na Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa kujengewa shule mpya ya Sekondari.

Akizungumza mbele ya Timu ya Watalaamu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais - TAMISEMI,  pamoja na Benki ya Dunia, mmoja wa wananchi kutoka Kijiji cha Chiponda, AmuriSeif Mchia amesema walikuwa na njaa ya shule ya Sekondari lakini sasa wameshiba.

"Sisi hapa Chiponda tulikuwa na njaa ya shule na sasa tumeshiba, watoto wetu walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 13 kwenda shule ya Sekondari Mnarani lakini kwa sasa wanatembea kidogo tu wanakutana na shule.  Tunaishukuru sana Serikali na tuko tayari kwa miradi mingine," amesema Mchia.

Ujenzi wa Shule hiyo umekamilika kwa asilimia 90  na imejengwa kupitia mradi wa SEQUIP kwa gharama ya Shilingi milioni 470.

Shule ya Sekondari ya Chiponda iko kwenye Kata ya Chiponda Tarafa ya Londo umbali wa kilomita zaidi ya 40 kutoka Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama mkoani Lindi.