Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kutambua mchango wa wadau kwenye Sekta ya elimu ni kuendelea kuhimiza Sekta binafsi na wadau kushirikiana na Serikali ili kufanikisha utoaji wa elimu bora nchini pamoja na mageuzi ya elimu.

Waziri Mkenda amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutambua mchango wa wadau hao ambapo amesema mageuzi ya elimu  yanahitaji mchango wa kila mdau ili kuyafanikisha.

 Amesema kuwekeza kwenye elimu ni nyenzo muhimu ya kusaidia nchi kwenda mbele na kwamba tofauti ya maendeleo ya nchi duniani haitokani na kuwa na mafuta, madini na rasilimali za asili bali inatokana zaidi na watu wake kuelimika na kuweza kutumia sayansi, teknolojia.
 
“Hakuna namna ya kukwepa kuwekeza kwenye elimu na kuwekeza kwenye elimu ni kuwekeza kwa vizazi na vizazi, kwa hiyo Rais wetu alivyoongeza fedha kwenye elimu haangalii uchaguzi ujao anaangalia kizazi kijacho,”amesema Prof. Mkenda.