Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema uwepo wa Samia Skolashipu imekuwa ni kivutio kuwahamasisha wanafunzi wenye uwezo mkubwa katika Sayansi kuendelea kusomea fani za Sayansi ambazo zinalenga kuchochea ustawi na maendeleo ya Taifa.



Akizungumza hii leo Agosti 26, 2024 katika halfa ya kuwapongeza Wanafunzi waliopata daraja la Kwanza katika Mtihani wa Kidato cha nne na sita Visiwani Zanzibar, Waziri Mkenda ameeeleza pis kuwa fursa za mikopo ya Elimu ya Juu zinatolewa kulingana na ufaulu wa Mwanafunzi.



"Katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maelekezo ya Rais, Samia Skolashipu inatoa ufadhili asilimia mia moja kwa wanaosomea nyanja za Uhandisi, Elimu Tiba, Sayansi, Hisabati na TEHAMA na niwahakikishie Mikopo inatolewa kwa kufuata vigezo vilivyowekwa" amesema Mkenda.



Amebainisha kuwa, Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha za Mikopo kutoka Bilioni 464 hadi Bilioni 757 na kwamba zitaendelea kuongezeka ili kuwezesha wanafuzi wengi wenye vigezo kupata elimu ya juu.