Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameitaka jamii kushiriki katika kudhibiti vitendo vya udanganyifu katika vipindi vya mitihani, ili kulinda heshima ya elimu na Taifa kwa ujumla.
Prof. Mkenda ametoa rai hiyo leo Novemba 30, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika Ufunguzi wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ambapo amesema wizi wa mitihani unaharibu maadili ya watoto na heshima ya taifa.
"Wizi wa mitihani si haki, naomba wananchi tushirikiane na Serikali kupiga vita vitendo vya udanganyifu, tudumishe uadilifu na kuwa wazalendo kujenga Taifa letu" alisema Prof. Mkenda.
Aidha Waziri Mkenda amelipongeza Baraza hilo kuendelea kusimamia kwa umahiri shughuli mbalimbali za Mitihani kwa kuzingatia sheria, sera na taratibu zilizowekwa, na kwamba hivi sasa limesaidia kukabiliana na changamoto ya udanganyifu katika Mitihani.
"Tuna kila sababu ya kujivunia kazi nzuri sana iliyofanywa na Baraza hili kwa Miaka 50 imesimamia mitihani kwa weledi mkubwa na limeisaidia serikali kuchuja na kufahamu umahiri wa wanafunzi" alibainisha Waziri Mkenda.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Said Mohamed amesema katika kuadhimisha Miaka 50, Baraza hilo limekutana na Wadau wa Elimu, kutathimini mafanikio, changamoto na kuweka maono kwa miaka ijayo kuendelea kuboresha utendaji kazi.
"Baraza limefanikiwa kwa ufanisi mkubwa kuendesha Kongamano la kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Wanataaluma kutoka sehemu mbalimbali nchini na wengine kutoka ng'ambo wameshiriki katika Kongamano hilo" alibainisha Dkt. Mohamed.
Aidha ameeleza kuwa Baraza pia liliendesha mafunzo kwa walimu wanataalum kuhusu namna bora ya kuandaa maswali ya umahiri.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hashimu Komba amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari kwa mkoa huo na sehemu nyingine nchini.
"Sisi tunajivunia mafanikio ya Baraza hili hasa katika kutekeleza majukumu yake jwa weledi, tutaendelea kushirikiana na NECTA kudhibiti vitendo vya udanganyifu.