
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Antony Kasore, amesema kuwa VETA itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na wamiliki wa viwanda na wadau wa sekta ya ufundi stadi ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya soko la ajira.

Akizungumza katika Mkutano wa Wamiliki wa Viwanda, Waajiri na Wadau wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi uliofanyika OKTOBA 17, 2025 jijini Dar es Salaam, CPA Kasore amesema kuwa maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanataka elimu ya ufundi stadi iwe shirikishi na yenye kuzingatia uhalisia wa mahitaji ya sekta mbalimbali.

CPA Kasore ameishukuru Serikali na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuimarisha miundombinu ya VETA na kuongeza vyuo vya VETA kutoka 37 hadi 80 vinavyofanya kazi, huku vyuo vingine 65 vikiwa katika hatua za kukabidhiwa.

Aidha, ameeleza kuwa VETA inaendelea kushirikiana na wadau katika kuandaa na kuhuisha mitaala ya mafunzo, sambamba na kuandaa mazingira ya mafunzo kazini kwa wanafunzi na wakufunzi.
“Tunahitaji wanafunzi wetu wafundishwe kwa vitendo, na wakufunzi wetu waendelee kupata ujuzi mpya, hasa katika maeneo yenye mabadiliko ya teknolojia,” alisisitiza

