Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kutoka Afrika Kusini Dkt. Bonginkosi Nzimande juu ya ushirikiano katika Nyanja za elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti.

Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Nzimande amemuomba Waziri Mkenda kukamilishwa kwa mapendekezo ya mkataba wa makubaliano kati ya Tanzania na Afrika Kusini kuhusu ushirikiano wa elimu ya Juu na Mafunzo ya Ufundi stadi.

Maeneo mengine yaliyopendekezwa na Waziri huyo kutoka Afika Kusini ni kuanzishwa kwa programu ya kubadilishana wahadhiri na wanafunzi kutoka nchi hizo mbili, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano ya kihistoria ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemhakikishia Waziri huyo kuwa wataalam wa pande zote mbili watakaa kwa pamoja na kupitia mikataba yote ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kukamilisha kwa wakati ili wananchi wa pande zote wanufaike na mikataba hiyo.