Walimu wanaofundisha masomo ya ufundi nchini wanapatiwa mafunzo ili kuwaongezea mbinu za kuweza kufundisha masomo hayo kwa umahiri.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mkoani Morogoro Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema Wizara ipo kwenye mageuzi makubwa ya elimu ili iweze kutoa ujuzi hivyo mafunzo hayo ni katika kuwajengea uwezo walimu wa kuenenda na mageuzi hayo ya elimu.

"Elimu ya ufundi lazima ikimbizane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hivyo walimu mnapaswa kuwa chachu kwa wanafunzi kuvutika na masomo hayo kupitia mbinu mnazotumia kufundishia,"amesema Prof. Mdoe

Prof. Mdoe amewataka walimu hao kuhakikisha wanatumia mbinu watakazozipata kuleta mageuzi katika ufundishaji wa masomo hayo na kuwafanya wanafunzi wapende kusoma masomo ya ufundi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya elimu ya ualimu Huruma Magheni amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo walimu wa ufundi kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika ufundishaji ikiwemo kutumia zana mpya kama vishikwambi na kompyuta ambavyo vilitolewa hivi karibuni kwa walimu nchini kote.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Walimu wa masomo ya ufundi walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa yatawasaidia kuboresha ufundishaji na hatimaye kuzalisha vijana wenye ujuzi.

Mafunzo ya walimu wanaofundisha masomo ya ufundi yanatolewa na Wizara kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu ( TESP) unaofadhiliwa na Serikali ya Canada