Serikali imedhamiria kuwarudisha Wasichana 12,000 walikatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali katika mfumo wa elimu kwa njia mbadala.
Hayo yameelezwa Januari 13, 2025 mkoani Morogoro na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizindua Warsha ya Tathmini ya Utekelezaji wa Mradi wa SEQUIP AEP, ambapo ameipongeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa kuendelea kuboresha elimu nchini.
Mkenda ameeleza kuwa mradi wa SEQUIP umeleta mapinduzi makubwa katika elimu ya sekondari, na kwamba Mradi huo wa thamani ya dola za Kimarekani milioni 500 unalenga kuboresha miundombinu ya elimu na kutoa mafunzo kwa walimu zaidi ya 29,300 wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati na kusaidia ujenzi wa shule mpya 830.
“Tunaendelea kutekeleza Sera Mpya ya elimu ambapo kuanzia 2027 elimu ya lazima itakuwa miaka 10. Hivyo, pamoja na miradi mingine, tunaendelea kuandaa miundombinu bora kuwezesha utolewaji wa elimu,” alisema Waziri Mkenda.
Warsha hiyo imewakutanisha pamoja watekelezaji, wasimamizi, na washiriki mbalimbali kutoka TEWW, ambapo mada zitakazojadiliwa ni pamoja na mafanikio, changamoto, na mikakati ya kutatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi wa SEQUIP AEP.