Serikali imetangaza kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakaonufaika na mpango wa ufadhili wa masomo kupitia Samia Scholarship, ambapo jumla ya wanafunzi 1,051 wanatarajiwa kupata ufadhili kwa mwaka huu wa masomo.

Akizungumza Julai 22, 2025, Jijini Dodoma na waandishi wa habari ,  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema ongezeko hilo linatokana na bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu ambayo imeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo wanafunzi 640 ndio waliweza kufadhiliwa.

“Kati ya wanafunzi hawa, 51 ni wenye mahitaji maalum waliopata daraja la kwanza katika masomo ya sayansi kwenye mtihani wa kidato cha sita,” alieleza Prof. Mkenda, “na wengine 1,000 ni waliopata ufaulu wa juu katika masomo hayo kitaifa.”

Ufadhili huo unalenga maeneo ya kipaumbele ya TEHAMA, Hisabati, Elimu Tiba, Sayansi na Uhandisi.

 Aidha, kati yao wanafunzi 50 watafadhiliwa masomo nje ya nchi katika maeneo ya Akili Unde (Artificial Intelligence), sayansi ya Data na  masomo yanayohusiana na fani hizo ambao pia watapaswa kuomba kupitia mpango maalum wa Samia Extended Scholarship AI/DS/AI+.


Amebainisha kuwa majina ya Wanafunzi wenye vigezo yanapatikana  katika tovuti ya Wizara na ike ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Waziri Mkenda pia amebainisha kuwa wanafunzi watakaomba ufadhili wa Samia Skolashipu Extended DS / AI + watapitia mafunzo ya miezi kumi katika kambi maalum ya maarifa ( Boot Camp)  itakayofanyika katika Taasisi ya Nelson Mandela ili kuwaandaa vyema kujiunga na programu hizo pamoja na masuala mengine muhimy ikowemo uzalendo.

Mpango wa Samia Scholarship umeendelea kuwa chachu ya kuwainua vijana kitaaluma na kuwajengea uwezo katika sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa kulingana na Dira ya Taifa 2050.