Timu ya Benki ya Dunia inayokagua utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) imepongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kujenga Kituo kitakachokuwa kikisimamia masuala ya watu wenye mahitaji maalum na jinsia.



Akizungumza Oktoba 29, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Timu hiyo ya Benki ya Dunia iliyoambatana na timu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Mtaalamu Mwandamizi wa Elimu kutoka Benki ya Dunia Nkahiga Kaboko amesema kituo hicho ni muhimu katika kutoa ujuzi na kuwajengea uwezo vyuo vingine ili kuboresha utekelezaji wa elimu ya juu jumuishi.



Mkurugenzi waTaasisi ya Taaluma za Jinsia Dkt. Lulu Mahai amesema kuwa kituo hicho kitawezesha UDSM kuwa mahali salama pasipo na ukatili wala unyanyasaji wa kijinsia na kuandaa wataalamu wa masuala ya kijinsia na Maendeleo ya Jamii.



Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Prof. Roberta Malee amesema amefurahi sana kuona maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na nia ya kuifanya elimu ya juu kuwa sehemu salama na wezeshi kwa wanafunzi wote na kwamba kitakuwa mfano kwa nchi nyingine.



Mwanafunzi wa Chuo hicho Mwenye mahitaji maalum ameishukuru Serikali kwani kupitia kituo hicho wanafunzi wote watapata elimu katika mazingira rafiki na bora



Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mbali ya kujenga kituo hicho, pia kinajenga Kampasi mpya Mkoani Kagera na Lindi, majengo mapya katika kampsi Kuu ya Dar es Salaam na katika kampasi ya Buyu kupitia Mradi wa HEET.



Aidha, kupitia Mradi huo Chuo hicho kimeandaa programu mpya za mafunzo, kimeanzisha kamati ya ushirikiano na viwanda na kupeleka wataalam masomoni ndani na nje ya nchi.