Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel E. Mushi, amemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, katika kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (Inter-University Council of East Africa - IUCEA)
Kikao hicho kilichofanyika Januari 15, 2025 Bujumbura, Burundi na kujadili masuala mbalimbali yanayohusiana na elimu ya juu katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu na kuwezesha wanafunzi na wafanyakazi kufanya masomo na kazi katika nchi mbalimbali za kanda hiyo.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na ulinganifu wa ada za vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, ufadhili wa wanafunzi na wahadhiri kusoma na kufundisha katika vyuo vikuu vya ukanda huo, pamoja na uanzishwaji na uendeshwaji wa vituo vya umahiri (African Centres of Excellence - ACEs).
Kikao hicho pia kilihusisha nchi nane (8) zinazoshiriki katika shughuli za IUCEA, ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudani Kusini, Somalia, Rwanda, na Burundi.