Serikali imeandaa Mfumo wa kidijitali wa taarifa za Shule (School Information System - SIS) ambapo walimu, Maafisa Takwimu pamoja Maafisa TEHAMA kutoka shule mbalimbali nchini wanapatiwa mafunzo ya mfumo huu.



Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo katika Mkoa wa Kagera, Afisa Elimu wa Mkoa Mwalimu Michael Ligola amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu mfumo huo kupitia ujuzi walioupata na kuwa mabalozi wa TEHAMA katika maeneo yao ya kazi.



Alisisitiza kuwa matumizi ya mfumo wa SIS yataongeza ufanisi katika usimamizi wa taarifa za wanafunzi, mahudhurio, na matokeo ya kitaaluma na kurahisisha mawasiliano kati ya shule, wazazi na wanafunzi.



“Mfumo huu unatarajiwa kurahisisha pia majukumu ya kiutawala na kitaaluma, na hivyo kuchangia katika ufanisi na ubora wa elimu,” alisema Mwalimu Ligola.



Washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuja na Mfumo huo na kuwapatia mafunzo huku waki ahidi kwenda kuendeleza mafunzo kwa walimu na watumishi wengine ambao hawajapata mafunzo katika ngazi ya Shule.



Mafunzo haya yamewezeshwa na Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), kwa lengo la kuhimiza matumizi ya TEHAMA katika mfumo mzima wa utoaji elimu na ujuzi.