Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.Wilson Charles Mahera ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuchangia maendeleo ya elimu ya wanawake katika Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Ubunifu ili kuwapa fursa ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii na viwanda.
Dkt. Mahera ametoa rai hiyo Septemba 22, 2024 wakati wa ufunguzi mbio za Nelson Mandela (Nelson Mandela Marathon) zilizoratibiwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ili kuhamasisha wasichana na wanawake kujiendeleza na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na ubunifu kwa ngazi ya Uzamili na Uzamivu.
Mbio hizo zimeongozwa na kauli mbiu ya "Jitihada kwa Sayansi, Hatua kwa Mafanikio", ambapo Dkt. Mahera amesema inaendana na dhamira ya Serikali kupitia taasisi ya Nelson Mandela inayolenga kukuza taaluma za Sayansi, Uhandisi, Teknolojia, na Ubunifu, ili kuwezesha kuzalisha bidhaa za uvumbuzi kwa jamii na viwanda.
Aidha Dkt. Mahera ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuandaa mbio hizo zilizowashirikisha watu mbalimbali wakiwemo wenye mahitaji maalum, huku akiwataka kuwa na muendelezo ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Maulilio Kipanyula ameeleza kuwa, mbio hizo zimeandaliwa kwa mara ya kwanza kwa lengo la kukuza ushiriki mkubwa wa wanafunzi wa kike katika elimu ya juu, hasa katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu, katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Ubunifu.
"Idadi ya wanafunzi wanawake katika taasisi yetu kwa ngazi ya uzamili na uzamivu ni asilimia 30, tunatamani idadi iongezeke hata kufikia asilimia 50, tukaona vyema kuwa na mbio hizi ili kuweka hamasa" alisema Prof. Kipanyula.