
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali inawetegemea wanasayansi na wahandisi ili kufanikisha dhamira ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda, amesisitiza kuwa kundi hilo lina mchango katika kuendeleza ubunifu, kuongeza tija na kuleta maendeleo endelevu nchini.

Prof. Mkenda amesema hayo Disemba 5, 2025 jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), akisema katika kutimiza azma hiyo Serikali imeendelea kuongeza fursa za mafunzo na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kusimamia ubora wa elimu sambamba na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023.

"Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mageuzi ya elimu, kwa kuwawezesha watanzania hususan vijana kupata maarifa, stadi na ujuzi ili kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi" Amesema Waziri Mkenda.
Amebainisha kuwa, Serikali kupitia mkopo nafuu wa Benki ya Dunia imewekeza jumla ya Dola za Marekani milioni tisini (90) ambapo kupitia fedha hizo Taasisi ya DIT, imeanzisha Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Mafunzo ya TEHAMA (RAFIC) katika Kampasi ya Dar es Salaam na Kituo cha Umahiri cha Uchakataji bidhaa za ngozi (CELPAT) kampasi ya Mwanza.

Ameipongeza DIT kwa kuendelea kutoa mafunzo bora, sambamba na kutambua, kujenga, kukuza na kuendeleza bunifu. Amesema kuwa Serikali inajivunia juhudi hizo na ameisisitiza kuendelea kusimamia majukumu yake kikamilifu.
"Sote tunafahamu kuwa, maendeleo makubwa ya kiuchumi yanatokana na matumizi mazuri ya elimu ya ufundi, sayansi na teknolojia" ameeleza Waziri Mkenda.
Prof. Mkenda amewapongeza Wahitimu wote, amewahimiza kuwa na ari ya kujiajiri, wawajibikaji na wazalendo.

